Saturday, December 12, 2015
Furaha huanza juu  na kumalizikia chini kama moto wa mshumaa,  na ikiwa chini hurejeshwa tena juu ili iangaze nafsi kama jua linavyoangaza dunia. Unakumbuka sio mara moja tumesikia furaha ikipotea.Baada ya muda inarudi?.Basi wakati ikipotea hujificha, ili simanzi itutawale , na  huzuni itufike. Tuwapo ndani ya hizi hali hujiona wapweke na hatufai kama tone la chozi mbele ya mvua . Ni upweke na uchungu huu ambao  nafsi hupitia , hatimaye mtu mmoja anadhamiria kuitafta furaha kwa gharama yeyote.Wakati mmoja akifanya haya, furaha huwa inarejeshwa juu taratibu ili uzito wa amani ukae mioyoni mwetu .Faraja na neema zije juu ya  amani. Pale furaha yote inaporudi huyo mtu atakuwa na sababu kubwa ya kuishi na kupendeza. Kwani sakafu ya moyo wake imepata kile ilichokosa kwa muda mwingi. Tabasamu la huyu mtu sasa lazima  ling’ae  Kuliko  hata nyota iwakayo saa nane za usiku.Ikiwa unataka usitengane na furaha unashauriwa kufuata njia zifuatazo

1.TUMIA FURSA.Ukitaka kuwa mtu wa furaha kila mara, usishindane na hali,usigombane na watu hata kubishana sana kwa sababu ya tukio fulani.Kwani siri ya furaha ni kuruhusu kila hali ije kama ilivyo na sio wewe unavyofikiria ni lazima iwe.Na kisha thubutu kuitumia kwa style na mbinu zako zote.


2.KUBALI UWEZO WAKO.Kwa maana ya kawaida uwezo ni ile nguvu ulionayo,kiasi cha fedha unachopata ,au idadi ya mali unayomiliki, Mitaji hii na mingine mingi  ni nyenzo kuu ya kukutoa sehemu moja  hadi nyingine.Kwani sisi husahau kuwa furaha haipatikani kwa kumiliki kila  kikubwa unachotamani, bali furaha huja kwa kuthamini kile kidogo ulichonacho toka mwanzo.

3.PENDA CHANGAMOTO.Kuna misemo ya kihindi isemayo kuwa  ''hata nyota isingeweza kun'gaa kama kusingekuwapo na giza'',''Hata mvua isingeweza kunyesha kama kusingekuwapo na joto''Ikiashiria kupata kitu kimoja ni lazima  kutambua mchango wa kitu kingine ambacho ni kibaya ama kizuri.Kwa maana  huwezi kuthamini ukimya kama hujawahi kusikia kelele na huwezi kuthamini furaha kama hujapata uchungu.Furaha ya kweli ni mbegu inayoota baada ya shina la uzuni kuanguka.mizizi ya chuki kung'auka.

4.TAFTA MAFANIKIO.Hapa usichanganye haya maneno mawili; mafanikio na ushindi.Ushindi ni dhana inayoambatana na  mapambano ama mashindano baina ya mtu mmoja na mwingine.Lakini mafanikio ni ile funguo ya furaha baada nguvu , fedha, mipango kufikia malengo ya juu.Haya malengo chanya ndio hatua kubwa unazopaswa kuzifikia ndani ya siku,wiki,mwezi n.k Kulingana na ulivyojiwekea.Mafanikio ni chakula muhimu kwa kila moyo  wa furaha.

5.CHAGUA MTAZAMO SAHIHI.Hii ni namna tunavyoangalia mambo.Ni jinsi tunavyofanana au kutofautiana na wengine.Chunguzi za masulara ya furaha zinasema.Mtu anayetizama kazi za mwenzake  kwa mtazamo chanya .Huambukiza furaha mara dufu zaidi ya mwingine atazamaye shughuri hizo kwa mtazamo hasi.Na tafiti ikaongezea kuwa kadri unavyotoa furaha kwa wingi ndivyo unavyopokea kwa wingi .

  
Thursday, November 12, 2015
Japokuwa kuna giza,mwanga,mwezi , jua , bado siku hazifanani.Kama hivyo ndivyo ni kitu gani hasa hufanana?.Siku zote wewe na mimi tumeumbiwa uhitaji.Kwa maana nyingine kila siku tunaongeza idadi ya vitu tunavyopenda,tunavyotaka. Vitu hivi vinaweza kutengwa  katika mipango na katika uchumi. Katika uchumi,mimi napenda  mshahara mkubwa.Bila shaka hupendi kuingiza pato dogo ,unapenda? .Haya mahitaji ya kifedha ni sehemu ndogo kati ya ile kubwa iundayo mahitaji yetu  ya msingi.Yaani malazi,makazi,chakula na mavazi. Katika upande mmoja ukubwa wa mahitaji ya msingi umepanuka kiasi cha kuziba  macho yasione mipango rahisi ya kujikwamua.Kwani tuzibwapo na kipindi cha njaa,usingizi,baridi n.k .Huwa ni ngumu kufikiria mipingo ya muda mrefu au ya kudumu itakayotuepusha  na taabu hizo.Na upande wa pili ni wakati unapokuwa huru husurutishwi na chakula, malazi, makazi, mavazi.Katika hii saa ambapo hatujazibwa na mahitaji tunaweza kuweka malengo, kuoata ndoto, kufanya mipango na kupendekeza mbinu. Hizi harakati na mipangalio   zinavuma tokea ndani ya mioyo yetu zikipita vichwani na kutua akilini. Akili ndio makao makuu ya kila ndoto,mipango na mbinu tulizojiwekea.Kwa kuwa hii sehemu ya ubongo ni mhimu kwetu kama nahodha ndani ya  meli.Basi tunapaswa kuitunza, kuiboresha na kuitumia   kwa uangalifu. Ahsanteh kwa watu  waliotufunza kusoma na kuandika, kwani kwa kitendo chao tumetambua akili hutiwa mwanga. Akili hutolewa gizani. Akili hubadirika. Akili hupokea maarifa kulingana na mambo yanayoizunguka.Na ili tufikie mahitaji ya kifedha na ya msingi tunapaswa kuwa waalimu wa akili zetu, tukizifundisha kulingana na somo zuri linalojiandika katika kuta za familia , mitaa, jamii na maeneo mengine tunayoishi.  Zikiwemo kata, wilaya , mikoa ,nchi ,bara n.k.Bila kuchukua mazuri ya sehemu uliopo akili hizi tunazilisha sumu .Itakayoua 'future' zetu .
Thursday, November 5, 2015
Kuna msemo wa miaka mingi usemao apandaye haba atavuna haba. Maana yake inaendana sambamba na maisha ya vijana wawili waliotoka familia tofauti. Mmoja ni Paul mwenye miaka 20 aliyetoka familia duni ,  na mwingine ni Michael mwenye miaka 21 aliyetoka familia bora.  Hawa vijana kulikuwa na kitu kilichoondoa tofauti zao. Hiki kitu ilikuwa ni kiu ya mafanikio. Kila mmoja alitamani maisha mazuri. Kulikuwa hakuna njia ya kupata hayo maisha bila kuhusisha wazazi wao. Paul alimwendea baba ake aliyekuwa mfugaji na mkulima akiomba maelekezo namna gani ataweza kufanikiwa. Baba ake  alimwambia mwanaye jambo asiloweza kutegemea. Hili jambo halikufanana na lile Michael aliloambiwa na mzazi wake. Michael alipomsihi baba ake,ampatie siri ya kupata mali na fedha kama zilizopo nyumbani. Mzazi wake alimcheka sana kabla hajasema yafuatayo. ''mwanangu mimi sikupata chochote toka kwa baba angu, babu yangu alisema kitu kimoja ambacho nataka usikisahau maishani mwako, sisi tumebarikiwa katika lolote tutakaloanzisha, likiwa sahihi utakuwa tajiri kama mimi ama marehemu babu yako''  Baada ya mazungumzo hayo Michael alianza safari ya kutafta maisha . Tukirudi kwa  Paul tunamuona  akianza safari ya maisha huku neno la mzazi wake likiwa kichwani na kumrudia mara kwa mara . Mzazi wake alimwambia kuwa ''mifugo na mashamba alionayo alipewa na baba ake,''  akasisitiza kuwa baba ake alisema ''wao hawakuumbiwa mafanikio  mengine wataendeleza mashamba na mifugo kwa kizazi hadi kizazi ''Lakini Paul hakuwa mtu wa kukata tamaa. Aliondoka kwao akaanza  maisha katika biashara. Biashara  ya kwanza ikafeli,  akafanya ya pili ikafeli,  ya tatu ikafeli, ya nne ika feli, Kabla hajaanza biashara ya tano .Paul  mwenye miaka 26 sasa  .alikumbuka kauli ya mzazi wake ''wao hawakuumbiwa mafanikio  mengine wataendeleza mashamba na mifugo kwa kizazi hadi kizazi'' ndipo akafanya hiyo biashara ambayo nayo kwa bahati mbaya ilishindikana. Paul aliketi chini na kutafakari kisha akarudi kwao  kuwa mkulima na mfugaji kama babu yake ,Huku kijana mwenzake( Michael) anatoka kwao na mtaji aliotafta mwenyewe anaanza na biashara ya kwanza inampa hasara, ya pili inamtia hasara , ya tatu inamtia hasara , ya nne inamtia hasara, ya tano inamtia hasara ya sita inamtia hasara ya  saba inafeli , ya nane inakwama ya tisa ina inajifunga, Katika Biashara ya kumi , Michael akiwa na umri wa miaka 30 anakumbuka maneno ya mzazi wake ''sisi tumebarikiwa,  katika lolote tutakaloanzisha likiwa sahihi umekuwa tajiri kama mimi ama marehemu babu yako'' na alipojaribu hii biashara ya kumi ikamfilisi. Lakini Michael hakati tamaa na mwisho anakuja kufanikiwa katika biashara ya 20 akiwa na umri wa mika 40 .Na kuwa tajiri kushinda hata baba  na babu yake.Kwani;

1. Ule muda wote wa makosa ulimjengea uzoefu na ujuzi mkubwa katika nidhamu ya fedha, uchumi na biashara.

2.Imani yake haikutetereka kwa maana hakuamini kwenye kushindwa 


3.Alijua hata kama huna kitu una nafasi ya kupata kitu kama tu bidii ni shina la utaftaji wa hicho kitu

4.Alibaini kuwa bahati sio kuzaliwa katika familia bora ama duni bali ni mwenyewe kuandaa mazingira yatakayopokea fursa na kuigeuza iwe ajira au mradi
.
5.Alipata ufahamu kuwa kuendelea sio lazima uwezeshwe, ukopeshwe, utaftiwe bali maendeleo yanaanza kwa chochote ulichonacho ikiwemo  wazo, elimu, nguvu , juhudi, akili,imani na bidii

6.Paul alishindwa kwa kuwa dira yake ilizimwa na maneno ya mzazi


7.Alikomea maisha ya kawaida kwa kuwa kauli ya mzazi ilitawala uwezo na mipango yake.


8.Paul hakuwa na mfano wa kuiga katika maisha zaidi ya babu yake mfugaji.

9.Kosa kubwa kuliko yote alilofanya Paul ni kitendo cha kukata taamaa.


10.Mwisho ,kufanikiwa ama kutofanikiwa ni matokeo ya sisi wenyewe tunavyosikiliza na kufanyia kazi mawazo na maneno ya watu wengine.
 
Wednesday, July 22, 2015
Nilipokuwa mtoto kuna kundi kubwa la marafiki walinizunguka. Mmoja wao alijulikana kwa jina la Pola. Mie na rafiki yangu pola tulishirikiana kwa ukaribu juu ya  mambo mawili.  Pola alipenda sinema za Anord Shwarzenegger , mimi  za Jack Chan.  Rafiki angu  asipokwenda kutazama sinema,  alipenda  kucheza mpira. Ambalo ni jambo la pili lililotunganisha . Pola akikusanya makaratasi, mimi nilifuma mpira . Ujamaa wetu uliwakasirisha watoto wengine. Wangefurahi kutuona tukitengana, huku Sinema na kandanda vikiwa kando na maisha yetu  kuliko   mbingu na ardhi.
                Baada ya kuandaa mipira . Ukitukosa uwanjani tupo juu ya miti tukifanya kile tulichoamini ni mazungumzo. Na watoto wengine walikiita kuwa ni mabishano.  Mada kuu ya maneno yetu ilikuwa ni sinema.  Pola alikuwa nimwingi wa furaha tukianza hizi mada. Bilashaka  sikuleta kilio mbele ya macho yake.  Kama yeye ambavyo hakuleta kero usoni mwangu.  Mazungumzo ghafla yalikata tuliposikia filimbi (priiii).  Kwa sababu ilikuwa ni saa ya kandanda, tuliteremka viwanjani tukiungana na watoto wengine wakiwemo maadui.  Kama marafiki wengi  wa utotoni , hatukucheza kandanda katika timu pinzani hata siku moja.  Daima tulikuwa wa timu moja. Kwa kipindi kile mechi hazikufika  mwisho  bila mtoto mmoja kuwa Mohamed ali,  akipiga    ngumi na mwingine  Van damme akipiga mateke. Waliopewa kipondo ni  wachezaji waliokuwa hawana kosa. Katikati ya tifutifu sikupendezwa kuona rafiki angu akipigwa , licha ya umri wa miaka 6 niliokuwa nao, niliamini ningelimtetea Pola (niliyemzidi mwaka mmoja) , kama kuku mdogo  anavyolinda kifaranga wake baada ya mwewe  kukaribia. Sijui nini humwingia pola , kwani wakati wa vurugu jamaa alitumia siraha kama Anord Shwarzenegger (kipenzi chake). Akianza kuwatupia mawe watoto waonevu . Na kuchapa fimbo  zisizo na mpangilio  . Vita ikifikia hapa Sikukimbia, niliwakimbiza,  sikuogopa niliwaogopesha kwa mbio na ujasiri kama Jackie Chan (kipenzi changu).
            Miaka ikaenda sote tukahitimu elimu ya msingi. Nikabahatika kuingia sekondari.  Akafanikiwa kufanya biashara . Miaka ikapita nikachaguliwa form six.  Akabahatika kuwa wakala wa vinywaji vya  kokakola. Miaka ikazidi kusonga. Nikajiunga na Chuo, Yeye akajiunga na miradi mikubwa . Nikasikia Pola kaoa na kufungua biashara  za Tv, DVD , CD na ving’amuzi. Muda ukapita , nikapata ajira ya ualimu, kitengo cha  michezo. Sijasikia chochote toka kwa rafiki yangu . Mtu tuliolindana wakati wa vita ,  leo muda wa amani tunatengana. Mtu aliyenifundisha umoja, ananiacha katika  utengano. Hua sikomei hapo kuwaza. Siku za likizo,  nikifuatilia tamthilia za kikorea ,kimarekani na Uingereza. Hujiuliza mswali yasiyo na majibu.  Tungekuwa na mawasiliano na Pola angempenda mastar kama jumong?, Angemfurahia Will Smith au Harry Potter?  Hakuna wa kujibu haya maswali miongoni mwetu .Sio mimi,wala wewe isipokuwa ni Pola tu.  Kabla na wewe hujampoteza rafiki ako kipenzi ,uliepitia nae hatua nyingi za ukuaji,mateso na raha,njaa na shibe,furaha na huzuni.Napenda ujifunze jinsi urafiki wetu ulivyovunjika.

1.sote tulikuwa busy

2.Mawasiliano yalikuwa magumu tukiamini itakuwa usumbufu mmoja kuwasiliana na mwingine

3.Kisha tulidhani mmoja kati yetu atakuwa wa kwanza  kumtamtafta mwenzake


4.Baada ya kipindi najiuliza kwa nini mimi tu ndo nianzishe mawasailiaano?

5.Hatukuonyeshana upendo tuliounyeshana  thamani zetu
6.Bila mawasiliano ni wazi kuwa kumbukumbu baina yetu ilizaliwa,ikakuwa na mwisho ikafa


7.Hatimaye  tukasauliana hadi leo

Wednesday, July 15, 2015
Miaka ya nyuma ilikuwa ni miongoni mwa nyumba nzuri hiyo sehemu. Mmliki wake ni bwana tajiri ambaye kila mmoja alimtazama kwa msaada. Gari ilikuwa ni kivutio cha kila jicho. Ilikuwa ni kama ndoto iliyotimia pale mmliki alivyoongeza gari na nyumba katika idadi ya miliki zake
               Lakini leo mali zote ni chakavu na kwa mujibu wa asili ya vitu, kimoja lazima kichoke ili kingine kije. Nyumba izeeke ili  nyingine ijengwe, gari lichoke ili  jipya linunuliwe. Je unadhani ni vyema kwa mtu wa namna hii , anayeishi na kumiliki hili gari la kale kuitwa mwenda wa zimu hivi sasa, na apelekwe mirembe au sehemu nyingine ya vichaa?
             Sidhani, kwa sababu  hakuna jipya chini ya jua. Nguo yako ya thamani ni dekio kwa mwingine, Salio lako la bank ni kiasi ambacho  mwingine anatoa msaada bure. Mrembo au mtanashati ulinaye leo   kaachwa na mwenzako jana. Hata dada anayeitwa kahaba pale mtaani au kule hotelini siku moja alikuwa bikira. Sasa ya nini majivuno? Maisha ni mafupi kujisikia, kujiona dhidi ya mwenzako. ’’Tungali wakosefu, hakuna mkamilifu’’  . Anasema steve job. Hakuna kitakachotusaidia wala sipendi kuona watu wakijikweza nakujivunia mali, uzuri, akili, kiwango cha elimu, umaarufu na  miliki za dunia. Mungu  anasema ’’Pendaneni na muongeze marafiki’’
                Siku zote kumbuka yule unayemdharau wakati unaelekea  juu ndo yule utakaye mkuta wakati unashuka chini.  Hivyo usiwe ni kisababishi  cha matatizo kwa mwingine. Kama utakuwa kisababishi ,  utakuwa umejipalia kaa la matatizo mwenyewe, na hakika , hao uliowaletea shida watakuwa  sehemu ya matatizo yako siku moja.
                 Mwisho  usisahau kuwa hata matawi ya mgomba  kuna siku huitwa  majani makavu. Hivyo hupaswi kupumbazwa na mali za duniani. Kwani siku moja zitachakaa na kufa.

                Endapo muda utafika ukahisi kulia,  basi niite, siahidi kukufanya ucheke siku hiyo,  lakini tutalia sote. Siku moja ukitaka kukimbilia mbali, usiogope, niite. Nakuahidi nitakimbia pembeni yako. Lakini ikitokea ukaniita na usisikie jibu, huenda  nakuhitaji.  Kwa maana siku  itakuja mmoja wetu hatokuepo tena. Na itakuwa umeshachelewa kusema ‘I care’. Machozi yatakuto lakini   haisaidii, nimeshatangulia mbele za haki. 
Tuesday, July 7, 2015
Mabadiliko ni kama maji huweza kuchukua umbo la sura yeyote. Na huweza kufuata uelekeo mmoja au zaidi. Ukitazama  sura ya teknolojia iliopo leo utabaini hii sio taswira iliokuepo jana, yaani miaka 20 iliyopita. Mageuzi haya yanatokea huku wagunduzi kuntu wakiwa ni miongoni mwa watu adimu katika hiki kipindi. Richa ya kukosekana kwa wagunduzi nguri wakiwemo; Isack Newton, Pythogrus, Edson Thomas,  kati ya miaka  1995 hadi 2015 . Kuna upepo wa mabadiliko unaoletwa na waboreshaji wanaofuata misingi ya hao wagunduzi kuntu. Wagunduzi dhahiri, wangunduzi halisi , wagunduzi waliovuma miaka yote.  Ndani ya hiki kipindi cha miongo miwili ( miaka 20 ).  Kuna wabunifu wanaochipukia na kumiminika kama utitiri.  Hawa ndio shina linaloshikilia urahisi wa maisha na urahisi wa mawasiliano katika dunia ya leo. Hali inayopelekea mambo yaliokuwa hayawezekani miaka 20 iliyopita kufanikiwa. Na hapa ni baadhi ya hayo mambo

1.IMO,SKYPE












Kitendo cha kuonana ana kwa ana baina ya watu wawili walio katika sehemu tofauti za mchi , ilikuwa ni kitendawili katika niaka ya 90.  Ahsanteh kwa teknolojia ya imo na skype kwa kuleta nyuso na sauti za watu karibu.  Wapendanao waliokuwa wametenganishwa na umbali,  masomo,  kazi na majukumu  ,sasa wanafursa ya kusalimiana na kutazamana kwa ukaribu kama pua na mdomo.

2.WHATSAPP
Ilikuwa ni rahisi  kwa mganga wa kienyeji wakati ule. Kuendesha majadiliano na watu anaowaona yeye tu , kama hiyo haitoshi aliweza kusema kitakachojiri  duniani kabla ya mimi na wewe kutambua lolote.Baada ya simu kuingia kila mtu kapatiwa uwezo huo. Tena kama ina whats app ndio mtajadiliana hadithi zote kuanzia; siasa , katiba, tamaduni , uongozi, ajira, michezo, burudani ,utabiri wa hali ya hewa,kubet n.k .Vyanzo vya hizi habari kwa mwaka 2015 sio tena ‘mafundi’ au waganga wa kienyeji  pekee bali ni rafiki zako,wanafunzi wenzako,wafanyakazi na jamaa uliohifadhi namba zao katika simu ya kiganjani mwako. Kwa kutumiana jumbe za sauti,picha na video  Whats app hukupa maarifa pamoja  na taarifa za hayo matukio mbalimbali


3.YOUTUBE
 1995,Televisheni ilikuwa ni kila kitu juu ya masuala ya video. Kuona ‘kichupa’ au video mpya ya msanii unayempenda ilikupasa utege jicho kwa luninga. Ukikosa tukio kubwa katika taarifa ya habari ulitakiwa kuwa mvumilivu hadi taarifa irudiwe, vinginevyo ungoje  kipindi maalumu au mwisho wa wiki. Hali sio hiyo tena miaka ya kuanzia 2005, na Shukrani za kipekee ziendee  youtube kwa kutupa uhondo wa video tulizokosa, tuzitakazo katika muda wowote, mahali popote na kwa mtu yeyote.  matukio makubwayaliokupita au uliyoyakosa katika tv utayapa hapa.

4.SHAZAM
Unakumbuka enzi hizo ukisikia mziki mzuri redioni, unatamani mtangazaji ataje jina la huo wimbo?. Ama unapita mahala kuna mdundo wa nyibo za ughaibuni,zinakugusa moyoni lakini hujui msanii wala jina la wimbo? Hii shida sasa imefika mwisho.Mwaka 2015 Kazi imerahisishwa sana .  Ni vyepesi zaidi ya kumsukuma mlevi. Kwa kutumia shazam unaelekeza tu simu au komputa karibu na mdundo wa nyimbo,  na ndani ya sekunde umeshapata jina la msanii na nyimbo 
.
5.GOOGLE EARTH

Zamani ilikuwa ni ngumu kufika pointi moja  bila kuwa na mwenyeji, bila kuuliza ama kupanda chombo cha usafiri. 2015 unaweza kutembea dunia nzima bila kukwea pipa, kuchukuwa treni, kupita na meli wala kupanda basi. Ikiwa una google earth na mji una ramani mtandaoni  , utaelekezwa  njia za kupita kwa mguu, kwa gari hadi sehemu za kuvinjari, hotel, supermarket, beach  na kona za afya ;  hospitali, zahanati, na maduka ya madawa baridi. Google hawatoi tu ramani bali pia vituo mhimu unavyotaka kujua
 .
6.FACEBOOK
Karibu kila mmoja ana damu ya uandishi. kubali!, kataa!. Kwa maana anafurahi kushirikisha jamii dhidi ya mafanikio  ,mipango, ndoto,  huku akitia moyo marafiki na kuomba msaada wa maombi kwa ndugu hata pongezi kuto kwa jamaa . Mmoja yupo huru kutoa mawazo na hisia zake mbele ya wengine. Hii sehemu ya maisha ya mtu mmoja dhidi ya wengine hufanyika kwa maandishi yanayoambatanishwa na picha nzuri ya mhusika. Kama ishara ya kujuza jamii nini kinachoendelea upande wake. Endapo hujui ninachojaribu kuelezea hapa,  nakusihi jiunge na facebook, ukashuhudie jinsi uhuru wa kujieleza ‘freedom of expression’ inavyotendewa haki. Ikiwa una kumbukumbu nzuri, pengine umebahatika kuishi na wezee katika miaka ya 90. Utaona  bibi na babu zetu hawakufaidi dhana nzima ya uhuru wa mawasiliano.Ukilinganisha na FACEBOOK

7.TWITTER
Nakumbuka nilisoma kitabu kimoja zamani kidogo, ambacho kilielezea namna wafalme walivyokuwa wakituma jumbe ulimenguni.Kitendo kilifanya na mtu mwenye mbio sana aliagizwa kupeleka nyaraka katika himaya nyingine , na hiyo himaya  iliteua mjumbe wao mwenye kasi sana mpaka falme ya tatu .Ambayo pia ilieneza habari katika falme ya nne. Mtindo uliendelea  mpaka falme ya sita ,saba hadi  ya mwisho.Na baada ya miaka habari ilienea ulimenguni kote. Stori ya hiki kitabu chenye maisha ya zamani, kinafunua muongozo wa teknolojia ya twitter . Kitu ambacho twitter hufanya japo ni ni ndani ya sekunde,au dakika tu. Ni kueneza habari kwa haraka, Hivyo miomgoni mwa matumizi mengi ya tweeter,  dunia nzima hujua nini kimejiri. Kwa kuendeleza habari husika iwe ni Alshabab, Sunami, mapinduzi, ongezeko la joto n.k  .Ndani ya masaa taarifa itakuwa imefika uchina, Marekani, uingereza, Brazil, Australia na Tanzania . Dunia nzima hupelekewa taarifa kwa kufanya swala endeleve linaloitwa ‘retweete’

8.INSTAGRAM
Wakati sote tunaamini bank ni nyumba ya pesa, ghala ni nyumba ya mazao na msitu ni sehemu ya miti.  Basi instagram ni nyumba au sehemu ya picha. Zamani kuona picha ya msanii, mtu maarufu au kiongozi mkubwa ilikuwa nadra,  mpaka utafte  gazeti au kutembelea maneo ya kazi zao. Ahsanteh Instagram kutuletea pozi, dizaini, mbwembwe na matukio mengi ya watu hawa katika mfumo wa picha.

9.EBAY, AMAZON, KUPATANA



Unakumbuka wakati unauza bidhaa na hakuna mteja? .Unataka kununua mali hakuna hakuna muuzaji?. Ilikuwa ni zama ya miaka ya 90. Kuanzia mwaka 2015 Ebay, Amazoni, Kupatana.com ( Tanzania )  inatoa uhuru wa kuuza na kununua bidhaa yoyote mtandaoni. Hapa utapata nyumba, mavazi,  usafiri, vitabu, mashamba n.k

10.HULKSHARE, SOUND CLOUD

Sauti ina thamani yake na ili hii haiba idhihirike haina budi kukusanywa pamoja katika mfumo flani. Miaka ya 90,   miziki ilitunzwa vyema katika santuri, kanda , cd na baadae miaka ya 2000 , zikaingia flash. Lakini ukisahau mbinu hizi . Hulkshare na sound clound ni mapinduzi makubwa miongoni mwa mengi katika kutunza, kusikiliza na kupakuwa au ku ’download’ sauti, nyimbo, midundo, mziki unayoipenda.


Monday, June 15, 2015
A.Y au Ambwene Yessaya ni mwanamziki mkongwe anayetetemesha bongo fleva likija swala la mafanikio.Msanii huyu kajiwekea mizizi mirefu hadi nje ya mipaka ya Tanzania.Akianzia na kundi la East Coast Army ,A.Y anapata umarufu kwa uwezo wake wa kurap vizuri,na baadae anajitegemea huku akifanyakazi na wasanii wakubwa kama Sean Kingstone,Romeo,n,k. Na hapa anakuuliza ''Ni kitu gani huwafanya watu wawe na mafanikio?'' kisha anasema ''Leo namalizia kukupa siri 10 ambazo ukizizingatia utabadilika na kuwa mtu ambaye kila mmoja atakuwa akikuangalia kama mfano.''Ambwene Yessaya(2015).

1. siri ya kwanza:UNAVYOFIKIRIA NDIO KILA KITU
Siku zote kuwa na mawazo chanya. Fikiria mafanikio na sio kushindwa. Kuwa makini na mazingira hasi. Siri hii inafaa kuwa ya muhimu zaidi kwenye orodha ya mambo ntakayokuambia.Imani kuwa unaweza kuyafikia malengo yako inapaswa kuwa imara. Pindi unapojiambia mwenyewe kuwa ‘siwezi..’, basi hautaweza. Mambo chanya huwatokea watu chanya.

2. siri ya pili:KUWA MSTAHIMILIVE NA JITUME
Mafanikio ni kama marathon na sio mbio fupi. Kamwe usikate tamaa. Ukimuuliza kila mtu aliyefanikiwa leo au ukisoma historia za watu wenye uwezo mkubwa kifedha na maisha kwa jumla, utagundua kuwa walijituma sana hadi kufika hapo walipo.
Hakuna njia ya mkato katika kufikia kilele cha mafanikio. Lakini kama unafanya kitu ambacho unakipenda – basi sioni hata kama unaweza kukiita ni kazi!

3. siri ya tatu: KUWA TOFAUTI
Kama utafanya kitu kile kile kama wengine wanavyofanya, ni ngumu sana kuwa na mafanikio. Ni muhimu sana kupata kitu tofauti na kukomaa nacho.Hivi ndivyo itakuwa rahisi watu kukuona na wewe kupata unachotaka. Iwe ni fedha, uhusiano wenye maana, mtu tofauti huvutia wote.

4.  siri ya nne: ANZA SASA
Watu wengi hushindwa kuufikia uwezo wao wa juu kabisa kwasababu huwa hawaanzi kufanya kitu. Siku zote wamekuwa ni watu wa kujiandaa, kujipanga na kusubiri muda mzuri wa kuanza.Kama ningeendelea kusubiri hadi leo pengine nisingekuwa na mafanikio haya niliyonayo. Kama nisingechukua hatua za kusafiri na kwenda Kenya, Uganda na kwingineko, nisingekuwa msanii ninayejulikana kama hivi sasa.Kama nisingekuwa mjasiri na kuamua mwenyewe kubadilisha video zangu na kuzigharamikia, naamini nisingewapa moyo wasanii wenzangu wanaowekeza sasa kwenye kazi zao. Kujiongeza ni neno sahihi hapa! Kama unataka kujenga nyumba, ni ngumu kupata kwa mfano shilingi milioni 50 za hapo hapo ili uanze. Anza kwa hicho ulichonacho mkononi na utashangaa kuwa una nyumba tayari! Si unaujua ule usemi kuwa hata mbuyu ulianza kama mchicha? 
Je unasubiri kitu fulani kabla ya kuanza? Ni kitu gani kibaya sana kinaweza kutokea kama ukianza sasa? Kama wewe ni mtu ambaye umekuwa ukisubiri muda muafaka ufike, acha kusoma post hii na anza kufanya kile umekuwa ukitaka kufanya. Post hii itaendelea kuwepo hapa hapa ukirejea tena. Ha ha ha ha! Tukutane kwenye siri ya tano! 

5. siri ya tano:ISHI KWA KILE ULICHONACHO/UNACHOINGIZA
Watu wenye uwezo huepuka sana kutumia hovyo fedha zao. Lakini cha ajabu, miongoni mwa wengi wenye kipato cha chini huishi maisha yaliyo juu ya uwezo wao. Hutumia zaidi kuliko kile wanachoingiza na hivyo kujikuta na madeni mengi. Kama wewe ni mtu wa aina hii, punguza sasa ili kujiwekea akiba kwaajili yako na familia yako.

6.  siri ya sita:KUJIWEKEA TABIA NJEMA ZA KILA SIKU
Tabia njema ni msingi wa kutengeneza utajiri. Tofauti kati ya watu waliofanikiwa na wale ambao hawajafanikiwa ipo kwenye tabia zao za kila siku. Watu waliofanikiwa wana tabia njema ama ili kueleweka zaidi niyaite mazoea mengi mazuri kuliko yale mabaya.
Kama unaelewa kuwa tabia zako mbaya zinakukwamisha kuwa tajiri, utambuzi huo utakuwa ni hatua ya kwanza katika kuboresha mienendo yako.
Kwenye kitabu chake kiitwacho ‘Rich Habits - The Daily Success Habits of Wealthy Individuals’, Tom Corley anakupa ushauri wa kuchukua karatasi na kuorodhesha tabia zako mbaya kwenye column moja na kisha zibadilishe kila moja kwenye column nyingi kwaajili ya tabia njema. Mfano ni kama huu:
Tabia mbaya
Ninaangalia mno TV Sikumbuki majina ya watu
Ninajizuia mwenyewe hadi kuwa na saa moja tu ya kuangalia TV
Ninaandika majina ya watu na kuyakumbuka
Watu wengi waliofanikiwa huyazungumzia mafanikio yao kwa kuwaongelea watu fulani waliowasaidia kuwaongoza kufika hapo walipo. Washauri (mentor) wamepitia njia unayohangaika nayo sasa na wanaweza kukuongoza kufika uendako wa haraka zaidi kuliko kama ukienda mwenyewe.
Kama unataka kuwa na afya njema, utahitaji kwenda kwa mshauri ambaye tayari ana afya. Kama unataka kuwa tajiri, basi pia mtafute mtu ambaye ni tajiri akupe baadhi ya siri zake.

Tabia njema
Kisha kwa siku 30, fuata maelekezo ya kwenye orodha ya tabia zako njema. Utashangaa namna utakavyofanikiwa.

7. siri ya saba:USIOGOPE KUOMBA MSAADA
Watu waliofanikiwa hawana kasumba ya kufa na tai shingoni kama mjerumani. Walipokumbana na vikwazo walitafuta msaada wa hali na mali kwa wale waliokuwa na nafasi kuwazidi.
Kila mmoja na ule uthubutu wa kufanya mambo yake mwenyewe, ni nzuri katika upande mmoja lakini pia mbaya katika upande mwingine.
Kama kuna mtu unamfahamu ni mjuzi kwenye sekta fulani na unahisi anaweza kukusaidia katika mradi wako sio mbaya ukimshirikisha katika ushauri.

8. siri ya nane:NI MARUFUKU KUKATA TAMAA
Safari ya kuyafikia mafanikio sio rahisi hata kidogo. Kama unataka kuwa na maisha mazuri kwa njia halali, ni lazima utakutana na vikwazo vingi ambavyo kama hutokuwa jasiri, ni rahisi sana kuanguka.Usikate tamaa pale mambo yanapokuwa magumu. Watu waliofanikiwa huvumilia. Hubadilisha njia. Hujaribu kitu kipya. Husonga mbele. Wanaweza kubadilisha muelekeo lakini huendelea mbele.

9. siri ya tisa:TAFUTA USHAURI KWA WATU WALIOFANIKIWA
Watu wengi waliofanikiwa huyazungumzia mafanikio yao kwa kuwaongelea watu fulani waliowasaidia kuwaongoza kufika hapo walipo. Washauri (mentor) wamepitia njia unayohangaika nayo sasa na wanaweza kukuongoza kufika uendako wa haraka zaidi kuliko kama ukienda mwenyewe.Kama unataka kuwa na afya njema, utahitaji kwenda kwa mshauri ambaye tayari ana afya. Kama unataka kuwa tajiri, basi pia mtafute mtu ambaye ni tajiri akupe baadhi ya siri zake.



10.siri ya kumi:JIWEKEE AKIBA
Wahenga walisema akiba haiozi na haba na haba hujaza kibaba. Watu wengi hudhani kuwa ili uweze kuweka akiba ni lazima uwe na kipato cha juu. Nakubali kabisa kuwa wakati mwingine watu hujikuta tukishindwa kutunza chochote kwasababu majukumu ni mengi kuzidi kipato chetu, lakini hebu chukua mfano huu:
Wakati ulipokuwa ukiingiza 50,000 kwa wiki, kwanini uliweza kuishi kwa hicho unachokipata na maisha yalienda? Kisha ulipokuja kupata 100,000 kwa wiki maisha yalibadilika kwa muda lakini baadaye ukaja kuona tena kuwa hiyo nayo haitoshi! Fundisho hapo ni kuwa binadamu hatuwezi kuridhika kwa kile tunachokipata na kwamba tunaishi kwa kile kinachopatikana.
Kwahiyo kama unaingiza 50,000 kwa wiki, ukifanikiwa tu kuweka 5,000 kwa wiki, kwa mwaka mzima utakuwa umeweka akiba ya 260,000! Lakini pia utaweza kujibana na kuishi kwa 45,000 iliyobakia.
Wengi wenu hapa mnapata zaidi ya hapa hivyo kama mkiwa na desturi ya kujiwekea akiba, hutaamini kiasi cha fedha ambacho utakuwa umefikisha baada ya mwaka mmoja au miaka mitano kwa malengo marefu zaidi. Anza sasa kujiwekea akiba.
Watu wengi waliofanikiwa huyazungumzia mafanikio yao kwa kuwaongelea watu fulani waliowasaidia kuwaongoza kufika hapo walipo. Washauri (mentor) wamepitia njia unayohangaika nayo sasa na wanaweza kukuongoza kufika uendako wa haraka zaidi kuliko kama ukienda mwenyewe.
Kama unataka kuwa na afya njema, utahitaji kwenda kwa mshauri ambaye tayari ana afya. Kama unataka kuwa tajiri, basi pia mtafute mtu ambaye ni tajiri akupe baadhi ya siri zake.
Je! Siri hizi 10 nilizokupa zimekufundisha au kukuwekea kitu kichwani?





Popular Posts