Sunday, August 24, 2014
Katika ukuaji wa mtu ndani ya jamii fulani, unashabihiwa na mambo zaidi ya manee , na ukuaji huo hautofautiani na ule wa mmea ndani ya msitu.Mmea hauchipui hadi kuwa hatua ya mti bila kuathiriwa na joto, mwanga, maji na udongo.  Usawa wa hivi viumbe hai ki makuzi unapatikana  baada ya mimea na watu kuzongwa  na athari za mazingira yanayozunguka viumbe vyote viwili . Haya mazingira mwisho wa siku ni sababu za unyoofu, uzuri, afya, stamina na maisha marefu ya  viumbe hao. Wakati mimea inakumbwa na athari zitokanazo na mazingira  kama hali ya hewa, rutuba, ardhi n.k .Binadamu anakabiliwa na  vipengele vitano vinavyoathiri maisha yake ambayo  ni ;familia, makundi,  shule, dini na vyombo vya habari. Vipera hivi   ni mizizi ya uelewa kwa binadamu , na huwa havifuatani kwa mtiririko na mpangilio maalum isipokuwa hutokea kulingana na muda pamoja na mahali mtoto anapoishi.
.1.Familia ni kitovu awali cha maarifa kwa binti ama kijana. Kupitia familia, watu hawa hujua dunia kwa mara ya kwanza katika hali mbili; ya kuishi na watu na jinsi  ya mapokezi . Ueredi unaosababishwa na vitendo vya kunakiri na kurudia wafanyavyo wazazi na ndugu wengine wanaowazunguka vijana .Marudio ni njia pekee kwa wanajamii wachanga kujaribu mienendo na maisha ya utu uzima. Kupitia mikono ya mama, baba,kaka ,dada , shangazi ,mjomba n.k , mtoto hukomaa kiakili na kimwili mpaka kujibu maswali mengi juu ya dunia.
2.Shule ni uwanja wa elimu unaofafanua mazingira, hali, historia,na maarifa  kuhusu mtoto anapotoka, alipo na atakapo kwenda. Mambo haya huwa katika masomo na  sehemu ndogo ndogo ambazo huitwa mada au topic .Kisha huandaliwa waelimishaji maalum ambao husimama baadala ya wazazi ili kufundisha  watoto hawa, ambacho ni kizazi kisichokuwa na maono pevu juu ya ulimwengu.Waelimishaji huitwa waalimu na na watoto  huitwa wanafunzi. Wakiwa shuleni huendelea kubadiri utafakali wa matukio, maada, watu na vitu kutokana na masomo mbalimbali wanayopata ndani ya taasisi hiyo.Hata wakiwa vijana, ambayo ni hatua kiasi ya ukomavu wa binadamu.Shule na taasisi nyingine za elimu  hupanuka kwa kujali umri na uhitaji ya huyu mwanajamii komavu.Kwa kumuelekeza afuate nini,aache nini,anapaswa kuifanyia nini jamii yake na kuafanua kwa kina taifa na dunia ni dhana zenye mantiki gani mbele ya uso wake.




..3.Makundi ni idadi ya wasichana ,wavulana na watu wengine wanaovutiwa  kuendesha jambo katika hali ya ushirikiano ,wingi na  umoja  . Kama msemo usemao'' onyesha rafiki zako nikueleze tabia yako''.Ndivyo makundi  huathiri ukuaji wa mtu mmoja. Katika makundi, marafiki wakikutana, watu wa rika moja wakionana, na  wenye umri unaoendana  wakijumuika, huathiriana mmoja baada ya mwingine hatimaye wote. Athari yake hujipambanua katika mazungumzo, hisia, ufahamu na mtazamo  wao.Hali inayotokea aidha wakiwa wanafahamu ama kutotambua mabadiriko hayo .Kama uzi wa mafuta unavyoshika moto kwa kasi, halikadhalika tabia ya mtoto mmoja hushika na kuenea kwa wenzake.Japo mara nyingi huwa ni jumla ya tabia za watoto ndani ya makundi zinazoathiri akili ya  mvula ama msichana mmoja.Endapo kundi sio jema mtoto hubomoka kwa kuwa na maadili mabaya na kundi likiwa bora kijana hujengeka kwa kuwa na tabia sitahiki .
4.Dini  ni kisima cha imani, chenye utamaduni na taratibu maalum kinachotoa mafunzo ya kiroho kuhusu mwenendo wa mtu na namna ya kukabiliana na ulimwengu  .Elimu ya kina hutolewa na watu maalum walioteuliwa kwa misingi na kanuni za dini na madhehebu tofauti tofauti.Huu  ni utaratibu ambao unashabaha ya kuwezesha  binadamu kupata mafunzo ya mambo yasionekana na yale ya kimwili.Wakati utaratibu wa kupata haya mafunzo hupitia kuabdu, kusali, ama kuswali ukiendelea. Dini huwa kama shule kwa kuwa na watu wa aina mbili, watu wanaofika ili kupata elimu  ambao huitwa waumini.Na wengine ni watu ambao hutoa hayo mafunzo, ambao pia hupewa majina kulingana na aina ya dini.Ndani ya dini mambo yasionekana ama kujificha huitwa  mambo ya kiroho. Huku yale ya onekanayo au  ya kimwili yakibakia kuwa ni kuvaa, kula, kunywa , kulala n.k. Hivyo waumini huenda katika madhehebu yao  ili kupokea maarifa juu ya mambo ya kawaida na yale ya kiroho.Muumini aendae kinyume na utaratibu uliopangwa huwa amefanya makosa ambayo hutambuliwa kama dhambi,ama maovu na kutakiwa kutofanya hayo makosa tena.Mwisho vijana waliokulia ndani ya dini huwa ni toauti na wale ambao hawakulelewa katika misingi hiyo.   
 




 5.Kipengele cha tano  ni vyombo vya habari , ambavyo huwa ni hatari na baraka kutegemea na  kijana na huduma za hivyo vyombo.Kijana atakuwa  katika  hatari inayotokana na vyombo kama redio, televisheni, magazeti, na mitandao (internet) pale atakapokosa misingi   endelevu ya kujisimamia.Ambayo inatokana na familia, ushauri mzuri wa makundi, elimu bora ya shule na mafunzo ya dini. Kwa maana vifaa hivi vya mawasiliano  huchukua  tamaduni, imani, lugha, sanaa, michezo na tanzu zote za maisha toka sehemu tofauti za dunia.Kama vile jamii za kisasa ,taifa lililoendelea, na mabara yenye hatua nzuri za kimaisha.Na kupereka katika jamii zinazoishi maisha ya kale na zama za nyuma.Vyomba vya habari hutoa picha za maendeleo toka ughaibuni kitu ambacho huwavutia  vijana wengi katika mataifa yanaendelea na kutaka kuwa kama hao wawaona katika sinema, magazeti,internet na mitandao mingine ya kijamii.Usishangea mavazi ya kileo,misemo ya kisasa,nyimbo ,mahusiano na miondoko ya vijana wa karne ya 21 .Hii ni sehemu yamapinduzi na athari zitokanazo na  vyombo vya habari tulivyonavyo chumbani,sebureni,mtaani na kwingine kote.
 

0 comments:

Popular Posts