Saturday, May 28, 2016
Ndoto sio tu kile kitu unachokiona uwapo usingizini bali pia ni kile unachotamani kukiona uwapo macho na kinakunyima usingizi.Ni mara nyingi miongoni mwetu tumekuwa na ndoto kadhaa.Kupunguza mwili,kupata kazi,kununua kiwanja,kuoa,kusomesha,kufanya biashara na mengineyo.Tuwazapo ndoto za aina hii  dhahiri  tunafungua vichwa kuwa vielevu,tunavisaidia kuwa komavu,tunaviwajibisha kuwa na busara halikadhalika hatuviepushi kuwa imara .Na njia kuu ya kutimiza ndoto yako ni pamoja na kufanikisha za wengine.Huku ukichukua masomo mhimu kutoka katika usumbufu na urahisi mmoja aliopitia.Ikiwa hapo juu tumeona ndoto ni kama mizizi inayoshikilia shina na matawi ya maisha yetu kwa maana zinagusa afya,ajira,makazi,familia,na uchumi, ni vigumu sana kutenganisha binadamu na ndoto,ndoto na binadam.Swali la msingi ni nini kifanyike ili ''kugarantee'' ndoto zetu? .Yapo mambo mengi ya kufanya ila hapa nakushauri kwa haya mawili matatu ya kuufanya ili ndoto itimie na kudumu milele.

1.ANZA HAPO ULIPO
Namna ndogo ya kukaribisha ndoto kubwa ni pamoja na kuanza kuona kila jambo gumu ni jepesi, kila linaloshindikana  linawezekana.Na namna tulivyo leo ni matunda ya maamuzi tuliofanya jana.Inawezekana tunasubiri sana,hatuamini mazingira yanayotuzunguka,au watu tunaoishinao.Lakini ukweli ni kuwa maisha ni popote.Dangote ni bilionea mwenye heshima duniani anayetokea Afrika sehemu iliyowahi kuitwa ni bara la giza.Facebook ni mtandao mkubwa  wa kijamii ulimwenguni lakini uliogunduliwa huko mabwenini. 

2.TUMIA ULICHONACHO.
Muumbaji wetu ni wa ajabu sana ,wakati wa kuumba binadamu hakumnyima cha kufanya.Kama huna mikono una macho,kama huna macho una miguu kama huna miguu una mikono,kama huna mikono una mdomo na kama huna kinywa basi una akili.Akimaanisha Usipocheza kikapu kama Jordan utakuwa Goal keeper kama Kaseja.Usipokuwa na Sauti ya kuimba kama Steve Wonder utakuwa mzungumzaji mzuri kama Nyerere.Na usipokuwa  ''genius'' kama Einstein utakuwa msomi kama profesa Lipumba.Usipokua mwandishi kama Shakespear utakuwa mtunzi kama Shaban Robert.Tumia ulichonacho na ndoto yako itimie.. 
3.FANYA UNACHOWEZA.
''Kwani wao weweze wana nini na sisi tushindwe tuna nini?''Ni swali alilouliza Juma Nature msanii mwenye ushawishi katika mziki wa kizazi kipya .Kinachopelekeaa mwingine kuweza ni mjumuiko wa makosa na masahihisho wanayofanya.Hutenda kiasi kidogo leo,kiasi kingine kesho na kingine tena kesho kutwa.Jumla ya utendaji huu kwa wiki,mwezi,mwaka ni mkubwa kiasi cha kutisha mtu mwingine .Na kila hatua mpya inakuwa  bora kuliko iliyopita.  

4.USIVUNJE SHERIA.
''Ukivunja sheria utapigwa tu'' Mizengo Pinda,waziri mkuu mstaafu aliwahi kusema.Hivyo akati tukitegemea neema kuu ndani na nje ya ndoto zetu hatuna budi kuheshimu kanuni na taratibu .Hasa zile zinazoongoza nchi,zinazolinda mtu na kutetea uhuru wa kila mmoja.katika umiliki  wa rasilimali.Sitegemei utimize ndoto kwa njia ya wizi,dhuruma,ukabaji,unyang'anyi na njia nyingine zisizo halali.

Popular Posts